islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


ALAMA ZA SIKU YA KIYAMA


29809
wasifu
siku ya kiyama ni siku nzito,na siku haina shaka kuwa itakuja,hakuna ane juwa siku hiyo si malaika alie karibu wala nabii alie tumilizwa,anaejuwa siku hiyo ni mwenyezi mungu peke yake,na siku hiyo kwa kuwa hakuna anae ijuwa lakini mwenyezi mungu ametutajia alama zake na mteme s.a.w kutuelezea baadhi ya alama hizo,na katika alama zake kuna alama kubwa kama vile kwa kutoka dajjal,na kuja kwa nabii issa a.s ,na kuna alama ndogo nao nikupotea kwa amana na kukudhiri uzinifu na kula riba.
Khutba ya

Shukran zote ni za Muumba wa mbingu na ardhi Mola wa watu wote rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad.

Katika khutba hii ya leo tutazungumzia kwa kina kumwamini Mwenyezi Mungu kikweli na siku ya mwisho pia tutahimizana kufanya vitendo vizuri na tutazindushana kukaribia siku ya kiama, vile vile nitahadharishe kutokana na fitna na njia za kujiepusha, na nimalizie kuzitaja alama za siku ya kiama.

Ama baada ya kumsifu Mwenyezi Muungu na kumtakia rehma na amani Mtume Muhammad. Ni vyema Muislamu yoyote popote alipo ajue kuwa nguzo za imani ni lazima na kuzifanyia vitendo vizuri. Katika nguzo za imani kuna kuamini siku ya kiama ambayo ni siku ya mwisho siku ya malipo na kabla siku hii haijafika kuna alama za kuonesha kwamba imeshakaribia. Na sio siri kwani zimesha dhihiri baadhi ya alama zake na haya ndio mazungumzo katika khutba yetu ya leo.

Enyi Waislamu watukufu! mazungumzo yetu ya leo yatahusu alama za kiama. Kwa hivyo ni vyema watu wajiandae na siku hiyo.

قال تعالى : (فَهَلْ يَنْظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَنْ تَأْتِيَهُمْ بَغْتَةً فَقَدْ جَاءَ أَشْرَاطُهَا فَأَنَّى لَهُمْ إِذَا جَاءَتْهُمْ ذِكْرَاهُمْ) [محمد: 18]

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala): {{Kwani wanangoja lingine ila kiama kiwajie? basi alama zake zimekwisha kuja, kutawafaa nini wakati kitakapowajia}} [ Muhammad : 18]. Ni lazima kwa kila muislamu kuamini siku ya mwisho alipe umuhimu mkubwa suala hili, kwani haikamiliki imani ya mtu mpaka aamini alama za kiama (kwani kuamini alama hizo ni katika kuamini siku ya kiama) ukizingatia kwamba Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alizitaja alama hizi na hakitasimama kiama mpaka zitokee alama hizi. Swahaba Hudhaifa ibn Asiid radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema: [ Tulikuwa tumekaa katika kivuli cha chumba cha Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) tukataja kiama na sauti zetu zikawa juu (mpaka Mtume akasikia) akasema : Hakitasimama au hakitakuwa kiama mpaka kupatikane kabla yake alama kumi].

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amebainisha ya kwamba siku ya kiama haijulikani ni wakati gani na wala hakuna anayejua isipokuwa yeye peke yake. Na hakumhusisha yoyote kukijuwa kiama si Malaika aliyekurubishwa wala Mtume aliyetumilizwa na Mwenyezi Mungu. Pia imebainishwa kwamba kiama kimekaribia wakati wake kama zilivyoeleza Aya za Quran Tukufu na hadithi za Bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

قال تعالى) : يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِنْدَ رَبِّي لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ ثَقُلَتْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَا تَأْتِيكُمْ إِلَّا بَغْتَةً يَسْأَلُونَكَ كَأَنَّكَ حَفِيٌّ عَنْهَا قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِنْدَ اللَّهِ وَلَكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ) [الأعراف: 187] Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala): Amesema: {{Wanakuuliza kuhusu kiama kitakuja lini? sema: ilimu yake iko kwa Mola wangu tu hakuna wa kudhihirisha wakati wake ila yeye. Imekuwa nzito mbingu na ardhi, hakita kuja kiama ila ghafla}} [Al-Araaf : 187].

وقال) : يَسْأَلُكَ النَّاسُ عَنِ السَّاعَةِ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِنْدَ اللَّهِ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ تَكُونُ قَرِيبًا) [الأحزاب: 63] Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala): {{Watu wanakuuliza kuhusu kiama kitakuja lini? sema: ilimu yake iko kwa Mola wangu tu. Na kipi kitakacho kujulisha lini kiama, pengine kiama kiko karibu}} [Al-Ahzab : 63]. Na pale Jibril alipomuuliza Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) kuhusu kiama Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akajibu: [hakuwa mwenye kuulizwa ni mjuzi kuliko anayeuliza» Aya na hadithi za Mtume rehma na amani zimfikie zinazoshiria kwamba hakuna anayejuwa wakati wa kutokea kiama isipokuwa Mwenyezi Mungu]. Vile vile mitume waliobakia hawajui wakati gani kiama kitasimama.

Kwa kweli Mwenyezi Mungu amebainisha wazi kwamba kiama kimekaribia na vile vile Mtume wetu Muhammad rehma na amani zimfikie ameweka wazi katika hadithi zake kwamba kiama kimekaribia sana.

قال تعالى :] (وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ تَكُونُ قَرِيبًا) [الأحزاب: 63]

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema kwenye Qurani Tukufu: {{Na kipi kitakujulisha lini kiama pengine kiko karibu}} [Al-Ahzab : 63].

قال تعالى) : اقْتَرَبَ لِلنَّاسِ حِسَابُهُمْ وَهُمْ فِي غَفْلَةٍ مُعْرِضُونَ) [الأنبياء: 1]

Mola (Subhaanahu wa Taala) Amesema: {{imekaribia watu hisabu yao (ya kiama) nao wamo katika kughafilika na wanalipuuza}} [Al-Anbiya : 1].

Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) asema: [ Nimetumilizwa na kiama kama vidole viwili]. Akashiria vidole viwili cha kati na cha shahada.

Ndugu mnaonisikiliza napenda kuwabainishia vigawanyo vya alama za kiama. Kwa hakika alama za kiama zimegawanyika vigawanyo viwili.

Alama ndogo.

Alama kubwa.

Alama ndogo ni zinatangulia au zinazokuja kabla ya siku kiama kwa mda mrefu na zinazoeleka na zinaweza kudhihiri baadhi yake pamoja na alama kubwa au zikaja baada ya alama kubwa.

Ama alama kubwa ni mambo makubwa ambayo yatadhihiri karibu na kiama na huwa si ya kawaida kwa mfano kuja Dajjal na nyenginezo.

Na ukizingatia kudhihiri kwake zimegawanyika vigawanyo vitatu

Alama zilizodhihiri na kuweko

Alama zilizodhihiri na bado zinatokea

Alama ambazo hazijatokea mpaka sasa.

Alama Ndogo za Qiyama:-

Ndugu zangu Waislamu napenda kuzitaja alama ndogo za kiama nazo ni kama zifuatazo;

- Kutumilizwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [ Nimetumilizwa na kiama kama vidole viwili]. Akashiria vidole viwili cha kati na cha shahada.

- Kufa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ni miongoni mwa alama ndogo za kiama, kwani ni ishara wazi ya kukatika wahyi kutoka mbinguni.

- Alama nyingine ya kiama ni kudhihiri fitna kubwa; itachanganyika haki na batili zitatikisika imani mpaka mtu ataamka asubuhi hali ya kuwa ni muislamu na atalala hali ya kuwa ni kafiri au atalala hali ya kuwa ni kafiri na ataamka hali ya kuwa ni muislamu.

Hii ni kuonesha kwamba mtu kuingia katika ukafiri ni wepesi kwa kule kuchanganyika haki na batili na ndio hali za zama zetu hizi, watu wamechanganyikiwa kiasi kwamba hawajui haki ni ipi na batili ni ipi. Na kila ikidhihiri fitna atasema haya ndio maangamivu yangu kisha itaondoka itakuja nyingine atasema muumini haya ndio maangamivu na na hazitawacha fitna kudhihiri kwa watu mpaka kiama kisimame. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Hakika kabla ya kiama kutakuwa na fitna kama kipande cha usiku wa giza mtu ataamka muislamu na atalala kafiri na atalala kafiri na ataamka muislamu na aliyekaa ni bora kuliko aliyesimama na aliyesimama ni bora kuliko aliyetembea na anayetembea ni bora ni kuliko anayekwenda mbio].

Katika alama ndogo za kiama ni kudhihiri moto katika ardhi ya Hijazi na kupotea amana. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Hakitasimama kiama mpaka utoke moto katika ardhi ya Hijazi unatoa mwangaza moto huo kiasi utaona shingo za ngamia Basra]. Hakika moto huu umeshadhihiri katikati ya karne ya saba mwaka 654 hijria na ulikuwa mkubwa waliweza kuuona wanavyuoni wengi ambao waliokuwa zama hizo na waliokuja baada yao katika kuuelezea moto huo.

Vilevile kupotea amana ni katika alama za kiama watu kutotekeleza majukumu waliopewa na kutowajibika inavyotakiwa, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) asema: [ Ikipotea amana ngojea kiama].

Katika alama za ndogo za kiama ni kuenea zinaa kiasi kwamba litakuwa jambo la kawaida na asiyejihusisha na jambo hilo watu. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Naapa kwa ambae nafsi yangu iko mkononi mwake hautamalizika umma huu mpaka asimame mwanamume na mwanamke na amlaze njiani afanye nae zinaa aseme mbora wao siku hiyo lau mtazunguka nyuma ya ukuta (mufanyie huko)].

Katika alama nyingine za kiama ni kuenea riba tukijua kuwa riba ni katika madhambi makubwa sana lakini namna itakavyoenea litakuwa jambo la kawaida, lakini watu hawajali na watajaza matumbo yao haramu.

قال تعالى) : وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا( [البقرة: 275]

Mola (Subhaanahu wa Taala) Amesema: {{Na Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na ameharamisha riba}} [Al-Baqara : 275]. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [ kabla ya kuja kiama kutadhhiri riba].

Miongoni mwa alama za kiama ni kudhihiri na kuenea muziki kwa wingi na watu watahalalisha miziki hiyo, Mtume ameeleza haya katika hadithi zake nyingi suala hili kwa hivyo inatakiwa Waislamu wachunge mipaka ya Mwenyezi Mungu kwa kuomba msamaha kwake na kutubia, kwani hali za wanaadamu ni mbaya na za kusikitisha sana. Huku tusisahau kupeana nasaha kwa kuamrishana mema na kukatazana yalio mabaya.

Miongoni mwa alama ndogo za kiama ni watu kujenga majumba makubwa na marefu tena kutoka kwa watu katika duni katika jamii kufikia kiwango cha utajiri na haya ni kwa mujibu wa maneno ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alipotaja baadhi ya alama za kiama: [ Ni kuzaa mtumwa wa kike bwana wake na utaona watu wasiokuwa na viatu waliouchi, masikini, wachunga mbuzi wanashidana kurefusha majumba]. Na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Hakitasimama kiama mpaka watu wajifakhiri kwa kujenga Misikiti].

Katika alama za kiama ni kukithiri uongo baina ya watu, watadanganyana kwa wingi huku tunajua kwamba uongo ni katika makosa makubwa Aliyoyakataza Mwenyezi Mungu katika Quran na vile vile Mtume rehma na amani zimfikie ameukataza uongo katia hadithi zake tukufu. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema katika hadithi yake: [ Hakitasimama kiama mpaka zidhihiri fitna, kukithiri uongo na kukaribiana masoko].

Vilevile hakitasimama kiama mpaka atamani aliye hai mauti kwa namna hali za watu zitakavyokuwa mbaya. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [ Hakitasimama kiama mpaka aende alie kaburini asimame aseme natamani mahali pako]. yaani atatamani alie hai afe yeye.

Kukaribiana masoko ni miongoni mwa dalili za kiama. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [ Hakitasimama kiama mpaka kukithiri uongo na kukaribiana masoko]. Hizi ndio miongoni mwa alama chache za kiama na ni vyema kwa muislamu yoyote azijue vizuri kwani akiziona huenda akajiandaa na siku ya mwisho kabla hajafikiwa na mauti kwa kufanya vitendo vizuri na kujiepusha na vitendo vibaya.

Khutba ya pili

Alama Kubwa za Kiama:-

Shukrani zote na sifa njema ni za Allah Mola wa viumbe na Mlezi wa viumbe vyote. Rehma na amani zimfikie Mwalimu wetu, Mtume wetu Muhammad.

Ama baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na vile vile kumtakia rehma na amani Mtume Mtukufu baada kutaja alama ndogo za kiama sasa katika khutba hii ya pili nitataja alama kubwa za kiama nazo ni kama zifuatazo:-

- Kutoka kwa Dajjal kiumbe wa ajabu ambaye atakaye wafitini sana watu na kuwapotosha sana na kuwatia katika ukafiri kwani atakuwa na pepo na moto, atakaye muamini yeye atamwingiza peponi na atakaye muasi atamtia motoni, ataendelea kufanya hivyo mpaka aje Nabii Isa aje apambane nae na kumuua.

- Miongoni mwa alama za kiama ni kutoka Yaajuj na Maajuj ambao watatokea Asia ya kati waliofungiwa kwa sababu ya uharibifu wao katika ardhi pale alipopita mfalme Dhul-Qarnain aliyewafungia na kuziba sehemu ambayo walitaka kutokea kupitia sehemu hiyo.

قال تعالى) : حَتَّى إِذَا فُتِحَتْ يَأْجُوجُ وَمَأْجُوجُ وَهُمْ مِنْ كُلِّ حَدَبٍ يَنْسِلُونَ ) [الأنبياء: 96]

Mola (Subhaanahu wa Taala) Amesema: {{Hata watakapofunguliwa Yaajuj na Maajuj wakawa wanateremka kutoka kila mlima}} [Al-Anbiya : 96].

قال تعالى) : قَالُوا يَا ذَا الْقَرْنَيْنِ إِنَّ يَأْجُوجَ وَمَأْجُوجَ مُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ فَهَلْ نَجْعَلُ لَكَ خَرْجًا عَلَى أَنْ تَجْعَلَ بَيْنَنَا وَبَيْنَهُمْ سَدًّا) [الكهف: 94]

Na Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala): {{Wakasema: Ewe Dhul-Qarnain hakika Yaajuj na Maajuj wanafanya uharibifu katika ardhi, basi je tukupe ujira ili utie baina yetu na baina yao kizuizi}} [Al-Kahfi : 94].

Katika alama za kiama ni kushuka Nabii Isa amani iwe juu yake atakuja kupambana na Dajjal ambaye alipotosha sana watu na Nabii Isa atamuuwa Dajjal.

Miongoni mwa alama za kiama ni kuja Mahdy.

Kuchomoza jua kutoka magharibi na wakati huo milango ya toba itafungwa na hatosamehewa mtu yoyote kuomba msamaha wala kurejea tena kwa Mwenyezi Mungu maneno haya yanatupa sisi changamoto ya kukimbilia kumuomba Mwenyezi Mungu na kurejea kwake, kwani mlango wa toba ukifungwa ufunguliwi na watu wataanza kuhesabiwa.

Kudhihiri moshi duniani na kutoka mnyama anaezungumza na watu na kuwakumbusha mambo ya Mwenyezi Mungu.

Kushikwa jua sehemu tatu; kushikwa jua mashariki, magharibi na bara arabu.

Kutoka moto sehemu ya Aden katika nchi ya Yemen ulio wazi kabisa utakaokusanya watu katika ardhi ya watu kuhesabiwa vitendo vyake. Utalala moto huo watakapolala usiku na mchana pia utalala watakapo lala.

Kwa kweli alama hizi kubwa tena za kutisha hatuna ujanja wowote wa kuzikwepa siku hii nzito na ya kuogopesha.

Enyi ndugu katika imani! Hizo tulizo zitaja ndizo alama za kuja siku ya mwisho ambayo ni siku ya hesabu watakapo hesabiwa watu wote, suala la kwamba je tumejiandaa kwa siku hii ni muhimu sana Je, tumefanya nini cha kutusaidia mbele ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)? Kwanini basi tusimtake msamaha Mwenyezi Mungu na kurudi kwake?.

Enyi waja wa Mwenyezi Mungu jueni ya kwamba kupatikana kwa alama ndogo za kiama kwa wingi ni dalili na ishara ya wazi ya kukaribia alama kubwa ambazo zitakapokaribia alama hizo kubwa ndio kuja kwa kiama chenyewe. Basi tumcheni Mwenyezi Mungu na tufanye amali nzuri na tujiandae vilivyo na siku hii ya mwisho. Na jueni ya kwamba kiama kitafika hakuna chembe cha shaka ndani yake.

Mwisho

Tunamshukuru Manani aliyetuwezesha kuwabainishia ndugu zangu Waislamu kumuamini Mungu na siku ya mwisho pia tumesisitiza vitendo vizuri na kutumia fursa vizuri kama ambavyo tumejitahidi kuwazindua waislamu kukaribia kiama, vile vile tumewatahadharisha waumini popote walipo kutokana na fitna na njia za kujiepusha tukamalizia kubainisha baadhi ya alama za kiama.

Mwisho tunamuomba Mwenyezi Mungu Atupe misimamo katika dini na kushikamana na dini mpaka mwisho wa pumzi zetu. Atujaalie miongoni mwa wanaofanya maandalizi mazuri ya kukutana naye siku ya kiama.





Vitambulisho: