islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


FADHLA ZA SIKU KUMI ZA MWEZI WA MFUNGO TATU( Dhul Hijjah)


17101
wasifu
Zama zenye baraka zaidi ni kumi la mwanzo la Mfungotatu, kwani lina daraja kubwa kwa Mwenyezi Mngu (SW) inayo onesha kuwa Analipenda na analipa daraja kubwa. Kumi hilo ni la masiku yenye baraka, yenye mema mengi, yenye maovu machache, yenye daraja za juu, aina mbalimbali ya mambo ya utiifu. Mwenyezi Mungu Ameyaapia masiku hayo, na Yeye Aliyetukuka haliapiijambo isipokuwa jambo kubwa. Na Ameyafanya masiku kumi hayo, ni bora wa masiku za duniani,kwa hivyo ni juu ya waislamu kuzidisha ibada na kujieka mbali na kumuasi mwenyezi mungu s.w.
Khutba ya

Mwenyezi Mungu Alipomuumba mwanadamu ili aje afanye ibada na Akaumba Pepo na Moto, kwa mwenye kutwii na mwenye kuasi. Akawawekea misimu ya ibada nyakati mbalimbali ili wazidishe thawabu waingie peponi kwa usahali.

Allah Anaumba na Kuchagua

Ama baada ya kumshukuru Allah (Subhaanahu wa Taala). Enyi Waislamu muogopeni Allah Ambaye Anaumba na kuchagua, kwa mfano ameumba mbingu na Ardhi na akajichagulia mbingu ya saba na Makka pakawa ni patakatifu akaumba pepo na Malaika, akaifanya firdausi ndio pepo ya juu zaidi, na Jibril ndiye kiongozi wa Malaika na katika mwaka akaweka miezi, siku, nyakati za siku na saa. Akachagua mwezi mtukufu wa Ramadhani, siku bora ni Ijumaa, usiku mtakatifu ni Lailatul Qadri, na saa ya kukubaliwa dua ipo Ijumaa na masiku matukufu yapo kwenye siku kumi za mwanzo wa mfungo tatu. Allah akawaumba wanadamu, akawachagua aliowathamini ni muuminina, na akawachagua katika muuminina mitume, akawapandisha cheo mitume fulani, akaita rusul, na katika rusul akawapandisha wengine wanajulikana ulul–‘azm, na katika hao akatubainishia vipenzi vyake, na bila shaka katika vipenzi vya Allah kiongozi wao ni Mtume wetu Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

Mu’min anaishi akiwa amebarikiwa

Muislamu alibarikiwa na Mwenyezi Mungu, aliwekewa madaftari mawili, moja kuandikiwa mazuri yake na jengine kuandikiwa mabaya yake. Ama kafiri aliwekewa daftari moja tu analoandikiwa mabaya tu. Ni juu ya Muislamu awe na lengo la kwenda peponi ajizatiti kiibada kila zama na awe na malengo kwa kila msimu, kwani Mola na Mtume walitueleza siri hiyo. Mungu (Subhaanahu wa Taala) amesema:

قال تعالى ) : مَنْ جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا) [الأنعام: 160]

{{Mja akifanya jema nitamlipa kwa hisabu ya mema kumi}}. Na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akaongezea: [Hata kama hakulifanya hilo jema lakini alitia nia pia atalipwa thawabu. Na aliyetia nia ya ubaya na akalifanya hilo ataandikiwa alifanya ubaya moja na Mwenyezi Mungu hamwangamizi ila atakayekuangamia]. Hivi ina maana ya kuwa twa-a ya Muislamu kwa Mola Muumba ina baraka kote kote, katika matamshi na vitendo vyake, ulimi wake umtaje Allah na kutaja mazuri mpaka kufa kwake, na yeye afanye mema mpaka awe na mwisho mwema. Maneno haya yametafsiriwa na swahaba, Maliki Ibn Swa’aswaa alikuwa akisema: “Vitendo vitano vya Muislamu, atalipwa malipo ya vitendo hamsini na saumu ya Ramadhani moja atalipwa miezi kumi, na siku sita za mwezi wa Shawwal, kila siku moja atalipwa siku kumi, kwa hivyo mwenye kufunga Ramadhani na siku sita za Shawwal ni kama aliyefunga mwaka.”

Ama sadaka, Mola atampa daraja mtoaji mpaka daraja mia saba. Na hijja isiyokuwa na makosa, malipo yake ni ya juu sana isipokuwa kustahiki Pepo. Twaa ni kisafisho cha kujisafishia dhambi, kama Mtume alivyofananisha swala na kuoga mara tano, jee atabakiwa na uchafu? Na kila ibada ina baraka zake.

Zama zenye Baraka zaidi kiibada ni Siku Kumi za Mfungo Tatu

Allah (Subhaanahu wa Taala) anavyotupendelea tupate thawabu zaidi, alitudokezea kuwa kuna siku kumi ambazo ni muhimu sana na akaziapia nazo, na Allah huapia kwa viumbe vitukufu au nyakati tukufu, au Ardhi tukufu. Kama mbingu na Ardhi, Alfajiri na Alasiri, au Makkah au akaapa kwa chochote Alichoumba.

Fadhila za Siku Kumi za Mfungo Tatu

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Alikutanisha ibada tukufu zaidi kwa wakati mtukufu zaidi, kwa mfano swalatul fajri na swalatul asri kwa nyakati zake ambapo wanakutana Malaika wa vipindi viwili na kuchanganikana na waumini, ndio Anaapa kwa Alfajiri na Anaapa kwa Alasiri. Mwenyezi Mungu Amezitukuza siku kumi hizi, ndani imo siku ya ‘Arafa, siku ya idd ya kuchinja na kadhalika. Na Amekutanisha swala ya usiku, na Yeye huteremka kila usiku, na Yeye amesema kwamba waja wema ni wale wanaoacha vitanda vyao wakaswali, kwa sababu ya kumuogopa Yeye, na kutaka pepo na mambo yao ya kilimwengu, Nami hapo usiku huwa nikiwauliza haja mbalimbali niwapatie, lakini kuna biri baina yao na shetani. Mmoja katika watu wema amesema: ‘Haikubakia ladha ya dunia isipokuwa swala ya usiku, na swala ya jamaa na kutangamana na watu wema’.

Ulikamilika uislamu katika siku kumi hizi, ambapo ndani yake kuna ibada mbalimbali na watu wakajitenga na maovu, ilivyokamilika Dini, ndio Sunna ikapata nguvu na bid’a ikavunjika. Allah (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

قال تعالى: (الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا( [المائدة: 3]

{{Leo nimewakamilishia Dini, na nimewatimizia neema yangu}}. Anasema Sahaba ‘Umar bin Khatwab: ‘Mimi naijua vizuri Aya hii ilipoteremka, iliteremshwa siku ya Arafa, siku ya Ijumaa, maswahaba wengi miongoni mwetu tukafahamu dini imekamilika na Mtume yuko safarini kuondoka’. Mmoja katika wanavyuoni wa kiyahudi anaelezea umuhimu wa siku hii na kuteremka kwa Aya hii nzito, “Lau kama ni dini ya kiyahudi, siku hii ingekuwa iddi ya kila mwaka.”

Kabla ya kuhuishwa tena uislamu, kulikuwepo na dini nyingi ambazo ziliwapeleka motoni kama vile ukiristo, uyahudi, umajusi na kadhalika. Lakini ulipohuishwa uislamu, dini zote ziliyayuka na uislamu ndio utakaobaki mpaka Qiyama, na siku hii ya ‘Arafa ndio neema ilipotimia na makafiri wakawa wamekatazwa wasiingie Makkah, Waislamu wakazidi kuwa kitu kimoja.

Kuna ibada zinazokusanyikana hapa, siku za hija, kuna swala, sadaka, kufunga sunna au kufunga kwa ambaye hakupata kuchinja, kuna dhikri na kadhalika mpaka imalizike hija.

Msimu wa ibada wa siku hizi kumi, haupatikani ila kwa mwaka mara moja. Dakika zake, saa, siku na wiki, ndizo zinazompendeza Mwenyezi Mungu, lau mwanadamu atajitahidi kiibada siku hizi, atakuwa amefaulu sana. Kwa hadithi iliyopokewa na Ibn ‘Abaas kuwa amesema bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Hakuna siku bora kwa Mwenyezi Mungu anazolipa thawabu nyingi kama siku hizi kumi. Wanafunzi wa Mtume wakamuuliza: hata kwenda jihadi?, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akawajibu: Hata kwenda jihadi, isipokuwa aliyetoka jihadi na mali yake, akafa huko na mali yake isipatikane ndio atakuwa ana thawabu nyingi kushinda huyu mwenye kufanya amali katika siku kumi]

Katika siku hizi kumi, siku ya tisa inajulikana ni siku ya ‘Arafa, inajulikana kwa thawabu na msamaha mwingi kutoka kwa Allah, ndio siku waumini wanapeleka dua zao kwa wingi. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Dua bora nzito ni ya siku ya ‘Arafa]. Na kwa sababu waumini wengi wameacha machafu yao kwa ajili ya ‘Arafa, mahujaji na wasiokuwa mahujaji na ndio siku ya hijja kubwa. Na mwenye kufunga siku hii husamehewa madhambi ya mwaka uliopita na mwaka ujao.

Ipo siku ya mwisho, siku ya kumi ya mfungo tatu, inayojulikana kuwa ni siku ya kuchinja, zipo ibada tofauti tofauti, kutupa vijiwe, kunyoa, kutufu, kukimbia baina ya Swafaa na Marwaa, kuchinja na kuswali Iddi.

Fadhila za siku hii ni nyingi. Muislamu anatakikana asizipoteze, bali azipatilize na ashindane katika mambo ya kheri na ajishughulishe kwa amali njema.

Khutba ya pili

Amali zinazokubaliwa kisheria

Baada ya himidi na kumswalia Mtume, katika amali zilizokubaliwa na sheria ni kumtaja Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Allah Anasema:

قال تعالى) : لِيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ فِي أَيَّامٍ مَعْلُومَاتٍ عَلَى مَا رَزَقَهُمْ مِنْ بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ) [الحج: 28]

{{Ili washuhudie katika hija manufaa yao na wamtaje Allah kwa wingi katika siku hizi maalum}}.

Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Katika Siku hizi tukufu mtajeni sana Allah kwa Tahliil na Takbiri na Tahmiid]. Hadith hii imepasishwa na Imam Ahmad.

Maswahaba wengi hasa wale wapokezi wa hadithi, baadhi yao ni Abu Huraira na Ibn ‘Umar, ilikuwa wakiona siku kumi zimeingia wakitoka mpaka sokoni, na wakipiga Takbiri, kila mtu kivyake na wale waliopo sokoni wakiitikia kila mtu kivyake na hapo ikishika kasi kila mtu huendelea na dhikri mbali mbali na wengine wanaendelea kusoma zaidi Qur’an, kwani kumtaja Allah mara kwa mara ndivyo anavyotaka Allah, ni njia ya kufaulu duniani na akhera, na ndio sababu ya kuhifadhika na ukafiri na shetani na moto mpaka Malaika humtaja mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa fulani ni mja mwema. Ndio silaha na amali bora ya kujisafisha na kupandisha daraja na kuongeza thawabu kwa wingi na kusamehewa kwa wingi, na Mizani inakuwa nzito. Kazi yenyewe ni hafifu na huzungukwa na Malaika na fadhila nyingi. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) amezishikanisha Swala na Dhikri, Mola (Subhaanahu wa Taala) Anasema:

قال: (فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلَاةَ فَاذْكُرُوا اللَّهَ( [النساء: 103]

{{Mukimaliza kuswali mtajeni Mwenyezi Mungu}}.

Na Amezishikaniza swala ya Ijum’aa na Dhikri, Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala):

وقال: (فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانْتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِنْ فَضْلِ اللَّهِ وَاذْكُرُوا اللَّهَ) [الجمعة: 10]

{{Naitakapokwisha Swala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Allah na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi}}.

Na ibada ya Hijja na dhikri Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala):

وقال) : فَإِذَا قَضَيْتُمْ مَنَاسِكَكُمْ فَاذْكُرُوا اللَّهَ كَذِكْرِكُمْ آَبَاءَكُمْ أَوْ أَشَدَّ ذِكْرًا) [البقرة: 200]

{{Na mwishapo kutimiza ibada zenu za hijja, basi mtajeni Allah kama mlivyokuwa mkiwataja wazee wenu”, na Saumu Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala):

وقال: (وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ( [البقرة: 185] {{Na kamilisheni hisabu hiyo, na mtukuzeni Mwenyezi Mungu}}.

Kuukaribisha Mwezi wa Mfungo Tatu

Katika amali tukufu ni kuukaribisha mwezi wa hajji kiibada na kujikurubisha kwa Allah na kufunga siku ya Arafa, kama Mtume (Subhaanahu wa Taala) alivyojibu: [ Inafuta dhmbi za mwaka uliopita na mwaka ujao].

Kuzidisha Amali za Sunna baada ya kumaliza za Faradhi

Kuswali sana Swala za Sunna baada ya kila faradhi kama Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alivyotufundisha nazo ni rakaa kumi na mbili. Na Swala za usiku nazo ni rakaa kumi na moja na Swala ya Dhuha na Swala nyenginezo. Kuhifadhi Sunna ni sababu ya kupata mapenzi ya Allah na mwenye kufaulu mapenzi yake anamuhifadhi, amjibu dua zake na humpa cheo.

Kutoa Sadaka kwa wingi

Katika siku kumi hizi Muislamu huzidisha kama vile ilivyo kwenye Saumu ya Ramadhani na Iddil adh-ha na mengineyo, kwani sadaka humuongezea thawabu nyingi na humpa kivuli siku ya Qiyama na humfungulia milango ya kheri na milango ya pepo na humpenda yeye Mwenyezi Mungu na humsafisha na madhambi yeye na mali yake na familia yake duniani na akhera.

Kufunga Siku Tisa

Muislamu azidishe kufunga katika siku hizi, sababu ni moja katika amali njema na lau atafunga siku tisa hizi imeruhusiwa na sheria. Imethibiti kuwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alifunga siku ya ‘Ashura na akasema atafunga na tisa. Na hapo ndani zipo siku nyeupe na hadithi zilizopokewa kuhusu kufunga huku ni nyingi sana lakini wanazuoni wa hadithi wanasema zikigongana hadithi mbili moja inathibitisha na nyengine inapinga basi tunaitanguliza inayo thibitisha.

Ibada ya Kuchinja

Siku kumi zikianza na mtu anataka kuchinja aendelee na ibada zake kama kawaida na ingawaje hakufika hajj lakini ajihisi yuko katika siku tukufu kwa hivyo asikate kucha, nywele, na kukata chochote kutoka mwilini mwake mpaka baada ya kuchinja mnyama wake, hivi ndivyo ilivyopokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na maswahaba zake, Mtume alikuwa akichinja wanyama wawili, mmoja ni wake na ukoo wake na mwingine ni wa ummati wake. Mwenyezi Mungu Atujaze sote na Atujaalie sisi ni katika wafuasi wake na atufufue na kundi lake na Atukutanishe naye peponi, yeye Mwenyenzi Mungu ni mpaji. Vilevile, ni muhimu kuzidisha kumswalia Mtume, kufanya hivyo humzidishia Muumini malipo makubwa kama alivyobainisha Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) katika hadithi zake.

Enyi ndugu katika imani, tushindane katika amali njema na dua na kutaka msamaha na tujikurubishe kwa Allah huenda ikawa ndio kufaulu kwetu na tuonyaneni na uvivu na dharau na tupatilize haya masiku. Ewe Mwenyezi Mungu Tuafikie utuongoze kimaneno na kivitendo na hakuna mwenye kutuafikia isipokuwa wewe. Ewe Mwenyezi Mungu Tuepushie maneno maovu na vitendo viovu na hawaa, na hakuna yeyote mwenye kutuepushia hayo isipokuwa wewe. Ewe Mwenyezi Mungu Tuongoze na utuelekeze kwenye usawa na Anibarikie mimi na nyinyi na aninufaishe mimi na nyinyi kwa Aya na utajo mtukufu na Atunufaishe kwa uongozi wa Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na maneno yaliyo sawa. Naomba msamaha kwa mola na nawaombea nanyi Waislamu mliobakia, nanyi jiombeeni kwani Mola wetu ni msamehevu sana na mwenye sikitiko.

Mwisho

Ndugu Muislamu, Usighafilike, Mwenyezi Mungu ndiye aliyekuumba hivyo ulivyo na akakuchagulia alichokuchagulia na akakupa nawe nafasi ya kujichagulia vile utakavyo, kuwa na moyo, uchume juani kwa muda mfupi na ukale kivulini kwa muda mrefu kwenye maisha ya milele, Allah ametudokezea misimu tofauti tofauti yenye malipo mbali mbali, kwa mfano, lailatul-Qadri na masiku kumi ya mfungo tatu. Tuzidishe ibada katika siku hizi kumi kwa kuswali, kufunga, kutoa sadaka, kuleta tasbihi, tahlili na mwisho kuswali idd na kuchinja.

Ewe Mweyezi Mungu, tujaalie tuwe waja wema, tupatilize kiibada hizi siku kumi, tufaulu. Na wajaalie waliokwenda hajj waende salama na warejee salama na hizi siku kumi zikiisha tuwe tumekuwa safi, hatuna madhambi. Amiin Wal-hamdulillahi.

 





Vitambulisho: