islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


kuhimiza ilimu na kuifanayia kazi


7097
wasifu
Ilimu ni nuru na uongofu. Na ujinga mi giza na upotevu. Ilimu pamoja na Imani ni utukufu duniani na akhera. Na kuifanyia kazi Ilimu ndio matunda yake, na ndio msingi wake na ndio lengo la Ilimu. Hivyo basi ni lazima kwa wanafunzi kuyafanyia kazi yale waliyoyasoma. Bila kufanya hivyo, Ilimu yao itakuwa ni hasara na maangamivu kwao. Mjuzi asiyetumia Ilimu yake ni kama mshumaa ambao unatoa mwangaza kwa watu na unajichoma nafsi yake.
Khutba ya

Ilimu ni msingi muhimu katika dini ya Kiislamu. Dini ya Kiislamu imejengwa juu ya Ilimu. Kwasababu Ilimu ndio mwangaza wa kuonyesha njia ya sawa na kuonyesha njia ya mbaya. Aya za kwanza alizo teremshiwa Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) zilikuwa ni za kufundisha ilimu, na kuhimiza Waislamu wafanye bidii kutafuta ilimu. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ 1خَلَقَ الْإِنْسَانَ مِنْ عَلَقٍ 2اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ 3الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ 4عَلَّمَ الْإِنْسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ) [العلق1: 5]

{{Soma, na Mola wako ni Karimu sana. Ambae Amemfundisha binadamu ilimu zote hizi kwa msaada wa kalamu. Amemfundisha mwanadamu mambo yaliyokuwa hayajui}}.

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Ametumia katika Aya hizo maneno kama; soma, ilimu, kalamu, kufundisha, yote haya ni kuonyesha umuhimu wa kutafuta ilimu kwa kupitia njia tofauti za kuweza kukufikisha wewe kupata ilimu hio. Katika Aya hizo kuna ishara ya kuonyesha kwanza kabla ya kufanya vitendo vingine ni lazima mwanadamu apate ilimu ili aweze kutekeleza vitendo vyake kwa ujuzi zaidi na maarifa ya kutosha kinyume na mafundisho hayo, basi mwanadamu atafanya mambo kwa ujinga na baada ya kupata faida na mambo hayo, atapata hasara tupu ima kwa kudhuru nafsi yake au jamii kwa jumla.

Wajibu wa kutafuta Ilimu kabla ya kila kitu katika Mafundisho ya Qur’an na Sunna

Katika Qur’an Tukufu,:

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

قال تعالى) : فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنْبِكَ) [محمد: 19]

{{Jua ya kwamba hakuna aabudiwaye kwa haki ila Mwenyezi Mungu, na omba msamaha kwa dhambi zako}}.

Amesema Imam Bukhari katika kitabu chake Sahihi Al-Bukhari: ‘Mlango unaozungumzia kusoma ilimu kabla ya maneno na vitendo’. Makusudio ya Imamu Bukhari ni kutafsiri Aya iliyotangulia ya kumaanisha ilimu mwanzo kabla ya vitendo. Ilimu imetangulizwa kwanza kabla ya kusema au kutenda, kwa sababu, ikiwa maneno na vitendo havikujengwa juu ya msingi wa Ilimu, maneno hayo na vitendo hivyo havina faida kwa mwenye kufanya. Khasara yake ni kubwa kuliko faida yake. Ndio Dini ya Kislamu kwanza ikatilia mkazo watu kusoma na kujuwa kabla ya kufanya vitendo.

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

وقال تعالى) : إِنَّمَا يَخْشَى اللَّهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ( [فاطر: 28]{{Hakika wanao muogopa Mwenyezi Mungu ni wanazuoni}}. Katika Aya nyingine Anasema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

وقال: (((وَمَا يَعْقِلُهَا إِلَّا الْعَالِمُونَ )[العنكبوت: 43]

{{Na hawafahamu mifano hiyo, isipokuwa wajuao}}.

Katika Sunna za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)

Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Kutafuta ilimu ni Faradhi juu ya kila Muislamu].

Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [ Mwenye kufuata njia kwa ajili ya kutafuta Ilimu. Mwenyezi Mungu atafanyia wepesi njia ya kuingia peponi ]. c) Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Mwenyezi Mungu akimtakia kheri mja wake humfundisha ilimu ya dini].

Muislamu hawezi Kufahamu Qur’an na Sunna za Mtume ila kwa Ilimu. Ni lazima kwanza ajilazimishe na kusoma ili apate ujuzi wa kufahamu. Bila ya kufanya hivyo, atakuwa ni miongoni mwa waliosifiwa na sifa ya ujinga. Ndugu katika Imani, haya ndio mafundisho ya Allah na Mtume wake, yameweka wazi umuhimu wa kusoma kabla ya vitendo. Kwa hivyo, Allah (Subhaanahu wa Taala) hatokubali kwa mja wake ibada au vitendo vilivyo fanywa bila ya ilimu. Kwa sababu hio, ndio Sheria ya Kiislamu ikaamrisha Waislamu kusoma na ikawa hukumu ya kusoma ni wajibu juu ya kila Muislamu.

Mambo Yanayo Lazimu Katika Kutafuta Ilimu:

Kuwa na Ikhlasi, nayo ni kusoma kwa ajili ya Allah (Subhaanahu wa Taala). Muislamu lazima awe na lengo kubwa katika kutafuta ilimu nalo ni kusoma kwa ajili ya kutaka raadhi za Allah (Subhaanahu wa Taala). Malengo mengine yanakuja baadae. Lakini, la msingi ni kusoma kwa ajili ya Allah (Subhaanahu wa Taala).

Kuchunga haki za Mwalimu, kwa kumuheshimu na kumsikiliza vizuri wakati wa kusoma na kuuliza masuali kwa njia ya heshima.

Kupanga mikakati ya kusoma, kwa kutanguliza ilimu ambayo ni muhimu sana. Mfano wa kusoma ilimu ya faradhi kabla ya ilimu ya sunna.

Kufanyia kazi ilimu, na kuwa na hisia ya jukumu kubwa ulilo libeba. Na kujuwa ya kwamba utaenda kuulizwa ilimu yako mbele ya Allah. Je ulifanyia nini?

Kufundisha watu. Ilimu ni amana kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Taala). Na ili tuweze kutekeleza amana hii kama anavyotaka Mwenyezi Mungu, ni lazima tufanye bidii ya kuwafundisha wengine wasio bahatika kusoma. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Mbora wenu, ni Yule aliye jifunza Qur’an na akafundisha].. Kwa hakika, ni jukumu kubwa juu ya wasomi kufanya bidii kuifundisha ilimu waliopewa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).

Khutba ya pili

Ndugu katika imani, tumeona umuhimu wa ilimu katika dini yetu ya kislamu. Na umma wowote hauwezi kuendelea bila ya ilimu. Waislamu waliweza kumiliki ulimwengu mzima kwa sababu ya ilimu. Leo Waislamu walipo achana na ilimu, au kuchagua baadhi ya ilimu na kuacha nyingine, kwa kudai hio ni ilimu ya makafiri, basi umma umerudi nyuma tumekuwa sisi ni wafuasi wa makafiri, badala ya makafiri kutufuata sisi.

Ndugu Waislamu, kuna umuhimu mkubwa wa kurekebisha nidhamu ya ilimu katika mashule yetu na madrasa zetu. Mfumo wa ilimu ulioko sasa wa kubagua ilimu ya dini na ilimu ya dunia, na kujenga fikra ya kuwa ilimu ya dini ni ilimu ya akhera, haina usaidizi wowote hapa duniani. Kwa hakika, hii ni fikra ya makafiri wenye falsafa inayo sema: Ya Mungu ya baki kanisani na ya Qaysar yatawale nchi. Waislamu wengi waliosomea nchi za magharibi wamejazwa fikra hizo, na baada ya kurudi wakaendelea kufundisha watu fikra potofu za makafiri. Wanazuoni wa zamani walikuwa wamekusanya fani za ilimu mbali mbali na kuweza kuongoza Umma katika Nyanja zote za kimaisha. Mfano wa wanazuoni hao; Imam Al-Ghazali, Ibnu-Rushdi, Ibnu-Al-Haytham, Ibnu-Siiriin, Ibnu-Taymiyah, Ibnul-Qayyim, na wengine mfano wao.

Mwisho

Ndugu Waislamu, Ni wajibu kila Muislamu kufikiria suala hili muhimu, na kuangalia njia gani nzuri ya kurekebisha nidhamu ya ilimu. Ili tuweze kuandaa kizazi ambacho kitakuwa na uwezo wa kusimamia Uislamu na kurejesha utukufu wa Dini ya Kiislamu katika ardhi. Marekebisho muhimu katika ilimu ni kama ifutavyo:-

Kurekebisha Manhaj (Mtaala) wa masomo, kwa kuandaa mtaala wa masomo kwa mtazamo wa Kiislamu

Kujenga vyuo vikuu kwa lengo la kuandaa Waalimu Waislamu wenye uwezo wa kufundisha Manhaj ya masomo kwa mtizamo wa Kiislamu

Kujenga Taasisi na Vituo vya Ilimu ya chini kwa wingi, ili watoto wa kiislamu wapate nafasi ya kusoma

Taasisi zote za jamii Kufanya kazi kwa ushirikiano kwa lengo la kuboresha ilimu katika jamii.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe kujitolea kwa ajili yake kwa kufanya marekebisho katika ilimu. Na Atuafikishe tuweze kuandaa Waislamu wa baadae watakao tumikia Uislamu kwa ikhlas na kujitolea kwa hali na mali.