islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


ZAKA NA KAZI YAKE KATIKA MSHIKAMANO WA KIJAMII


7871
wasifu
Katika vitu vikubwa alivovipasisha Mwenyezi Mungu katika mali ni Zaka ambazo ni nguzo ya tatu katika nguzo za Uislamu, na zinakwenda sambamba na Swala katika Qur'ani yenye hukumu zilizothibiti. Mwenyezi Mungu Amezifaradhia kwa hekima kuu. Hakuzifaradhia ili kuchukua kwenye mali ya waja, lakini ziwe ni zenye kusafisha mali yao kwa kuwakunjua mafukara wao, iwe ni sababu ya wao kupendana kwa kusaidiana na kushikamana kijamii, wao kwa wao.
Khutba ya

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) na Anayestahiki shukran za dhati. Pia rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

Je, waijua ibada ya kutoa mali yako wewe Muislamu? Je, wajua kwamba ibada hii ukiifanya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Atakuzidishia baraka katika mali yako hapa duniani na malipo makubwa kesho Akhera? Je, hujui kwamba mali uliyonayo ni mali ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) na Amekupa mtihani katika mali hayo? Je, watarajia kufaulu mtihani huo?.

Enyi waja wa Mwenyezi Mungu! tutazungumzia katika khutba yetu ya leo kuhusu ibada iliyo tukufu ambayo mtu inaambatana na mali. Mtu akitioa mali yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala), mali yake huzidi na kupata malipo makubwa kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) na ni nguzo ya tatu katika Uislamu si nyingine nayo ni zaka. Ni wajibu wa kila Muislamu mwenye mali yaliyofika kiwango kutoa fungu maalum. Mola (Subhaanahu wa Taala) amesema ndani ya Qur’an tukufu:

قال تعالى) : وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآَتُوا الزَّكَاةَ) [النور: 56]

{{Na simamisheni Swala na mtoe Zaka}}. Na katika hadithi za Bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Uislamu umejengwa na mambo matano; kupwekeshwa Mwenyezi Mungu, kusimamisha Swala, kutoa Zaka, kufunga mwezi wa Ramadhani na kufanya hija].

Yamekuja maonyo mbali mbali na tahadhari kwa Muislamu katika suala nzima la kuikwepa Zaka na kufanya ubakhili wa kutekeleza ibada hiyo. Mola (Subhaanahu wa Taala) ameahidi adhabu kali kwa kila ambaye haitekelezi ibada hii tukufu. Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala) :

قال الله عز وجل) وَمَا لَكُمْ أَلَّا تُنْفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَلِلَّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَا يَسْتَوِي مِنْكُمْ مَنْ أَنْفَقَ مِنْ قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ أُولَئِكَ أَعْظَمُ دَرَجَةً مِنَ الَّذِينَ أَنْفَقُوا مِنْ بَعْدُ وَقَاتَلُوا وَكُلًّا وَعَدَ اللَّهُ الْحُسْنَى وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ) [الحديد: 10]

{{Na wala wasidhani wale ambao wanafanya ubakhili katika yale aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni bora kwao. La ni vibaya kwao. Watafungwafungwa kwa yale waliyofanyia ubakhili Siku ya Kiama, na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ana khabari za yote mnayoyafanya}}. Vile vile Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) :

وقال تعالي : (يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا إِنَّ كَثِيرًا مِنَ الْأَحْبَارِ وَالرُّهْبَانِ لَيَأْكُلُونَ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَيَصُدُّونَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنْفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَبَشِّرْهُمْ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ34 يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنْفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنْتُمْ تَكْنِزُونَ ) [التوبة34: 35]

 

{{Na wale wakusanyao dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Mwenyezi Mungu, wape habari za adhabu inayoumiza. Siku mali yao yatakapotiwa katika moto wa jahannam, na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao (na huku wanaambiwa). Haya ndiyo (yale mali) mlio jilimbikizia nafsi zenu basi onjeni (adhabu) yale mliyokuwa mkiyakusanya}}.

Faida za Zaka kwa upande wa Dini

Ndugu zangu katika imani! Zaka ina faida nyingi sana, nyingine za kidini, za kitabia na pia faida za kijamii. Basi kaa makini nikutajie miongoni mwa faida zake za kidini:

Kutoa Zaka ni kusimamisha nguzo, katika nguzo za Uislamu ambayo ni sababu ya utukufu duniani na kesho akhera.

Zaka zinamkurubisha mja kwa Mola wake na zinamzidishia mtu imani.

Mtu atoapo zaka hupata ujira na malipo makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Asema Mola (Subhaanahu wa Taala):

قال الله تعالى): يَمْحَقُ اللَّهُ الرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ)

{{Allah Anaiangamiza riba البقرة: 276] na Anaikuza sadaka}}.

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) humfutia madhambi Muislamu atoapo zaka. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) Amesema: [Na sadaka (zaka) inaondosha maovu kama maji yanavyozima moto].

Faida za Zaka kwa upande wa Tabia

Na miongoni mwa faida za kitabia:

Kutoa zaka inamuweka mtu katika kundi la watu wakarimu na wenye kujali maslahi ya watu,

Kutoa zaka kunamfanya mtu kusifika na sifa ya huruma na upole kwa ndugu zake.Kwani Waislamu wenye huruma Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) pia huwahurumia.

Kutoa zaka kunasafisha vifua vya watu wenye kupewa mali ile na watampenda mtoaji kwa kule kuwajali ndugu zake na kuwasaidia.

Kutoa zaka kunamsafisha mtoaji na sifa ya ubakhili na uchoyo. Na tabia mbaya hii ya ubakhili ni miongoni mwa tabia mbaya ambazo haitakiwi Muislamu kujipamba nayo. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema katika kitabu chake kitukufu:

قال تعالى: (خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِمْ بِهَا( [التوبة: 103] {Chukua katika mali yao zaka ili uwasafishe na uwatakase}}. Kuwatakasa na kuwasafisha kutokana na tabia ya ubakhili.

Faida za Zaka kwa upande wa Jamii

Na miongoni mwa faida za kijamii katika kutoa zaka:

Kutoa zaka huwaondolea watu matatizo ya kiuchumi waliyonayo na kama illvyo ni kwamba wanaohitajia ni wengi.

Kutoa zaka hutilia nguvu mambo ya Waislamu wanayotaka kuyafanya kwa mfano kupigana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).

Zaka huondoa chuki baina ya maskini na matajiri na kuleta mapenzi baina yao.

Zaka hukuza mali na kuyazidisha na kuwa na baraka. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Haipungui mali inayotolewa zaka].

Kutoa zaka hueneza mali baina ya watu na haibaki kwa matajiri bali huzunguka kati yao.

Na hizi faida tulizozitajaza ziwe ni za kijamii au za kidini au za kitabia zinaonesha kwamba kutoa zaka ni jambo muhimu sana na dharura Ili kutengeneza nafsi ya mtu na jamii kwa ujumla.

Enyi watukufu Waislamu! kutoa zaka kuna athari katika nafsi ya mtu na jamii kwa ujumla. Kwani kutoa zaka ndio nidhamu ya kwanza waliyoijua watu katika kuwasaidia wanaohitaji na uadilifu katika jamii nzima ya kiislamu. Kwani mali inatoka katika tabaka ya matajiri na kwenda katika tabaka ya maskini na wanaohitajia. Ukweli ni kwamba zaka inasafisha mali ya mtoaji na kuikuza kama ambavyo inamtakasa moyo wa mtoaji zaka kutokana na tabia ya ubakhili, tamaa na kutojali wanaohitajia. Vilevile inasafisha moyo wa anayepewa zaka kutokana na tabia mbovu ya uhasidi na chuki kwa mwenye mali.

Tukiangalia vyema pia kutoa zaka kunazidisha mshikamano kati ya jamii inayoishi pamoja na kuondoa umaskini na pia kuangamiza matatizo ya kijamii, kiuchumi na ya kitabia endapo itatolewa na kupewa wanaostahili.

Khutba ya pili

Mali yanayotolewa Zaka

Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Muumba wa mbingu na ardhi. Rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

Enyi waumini! mnaonisikiliza napenda kuchukua fursa hii adhimu kuwatajia mali ambayo inatakiwa kutolewa zaka kwa lengo la kukumbushana. Miongoni mwa mali ambayo hutolewa zaka ni dhahabu, fedha kwa sharti ifike kiwango na wajibu ni robo ya kumi ya dhahabu au fedha.Na katika mali ambayo ni lazima kutolewa zaka ni bidhaa za biashara nazo ni kila kilichofanyiwa biashara kwa mfano:majumba, magari, nafaka, mifugo, vitambaa na vyingenevyo. Na ni wajibu kutoa katika mali tuliyo yataja robo ya kumi.

Ama vitu vilivyoandaliwa kwa matumizi ya kawaida kama Magari ya matumizi, Majumba ya kuishi na vitu mfano wa vitu hivi havitolewi Zaka. Kwa neno la Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Haifai Muislamu kumtoa mtumwa wake wala farasi wake zaka].

Baada ya kuwaelezea mali ambayo yanayotakiwa tutoe Zaka na mali ambayo hayafai kuyatoa zaka. Sasa nachukua nafasi hii kuwatajia wanaostahiki kupewa zaka hizo. Miongoni mwa watu wanaostahiki Mwenyezi Mungu aliyetukuka ndani ya Qur’an Tukufu Aliposema :

قال تعالى) : إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّهِ وَاِبْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِنَ اللَّهِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ) [التوبة: 60]

{{Hakika zaka hupewa mafukara na maskini na wanazikusanya na waliosilimu karibu na watumwa na wenye madeni na katika jihadi na kupewa msafiri zaka hii ni faradhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikma}}.

Nachukue tena nafasi hii kuwafafanulia aliyowataja Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) katika wanaostahiki kupewa zaka.

Wanaostahiki Kupewa Zaka

Fukara; ni mtu ambaye hapati cha kumtosha isipokuwa kidogo chini ya nusu.Kwa hivyo ikiwa mtu hapati cha kujisimamia yeye na familia yake nusu mwaka basi huyo ni fukara. Kwa hiyo atapewa cha kumtosha yeye na familia yake mwaka mzima.

Maskini; ni mtu ambaye anapata cha kumtosha nusu na zaidi lakini hapati cha mwaka mzima kwa hiyo hupewa zaka ili kumkamilishia mahitaji.

Wenye kukusanya zaka; ni wale ambao wanamuwakilisha kiongozi kwa kukusanya mali ya zaka kutoka kwa wenye mali na kuwapelekea wanaostahiki na kuyahifadhi.

Waliosilimu karibu hawa hupewa ili kuzitia nguvu imani zao hatimaye wawe walinganizi wa dini ya kiislamu na kuwa mfano mzuri.

Mtumwa; anaingia katika tamko hili ni mtumwa ambaye husaidiwa kujikomboa kwa mali ya zaka.

Wenye madeni endapo hawana cha kulipa madeni yao na wenye madeni watapewa kile cha kulipa madeni yawe madeni yao ni mengi au machache.

Hata kama wanao uwezo wa kujitafutia chakula lakini hawezi kulipa.

Kutoa zaka katika jihadi; hutolewa katika jihadi kinachowatosha wapiganaji katika vita kununulia silaha na matumizi mengine ya kivita.

Msafiri; ni msafiri aliyekatikiwa na safari. Msafiri hupewa mali ya zaka ili ziweze kumfikisha mjini kwake anakokwenda.

Na hawa ndio ambao Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amewataja kwenye Kitabu Chake, na Akaelezea kwamba ni lazima kutekelezwa ibada hii kwa ajili yake. Wala haifai kutolewa zaka katika sehemu nyingine kwa mfano; kujenga Misikiti, kutengeneza njia, kuchimba visima na mengineyo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu Amewataja Mwenyewe wanaostahiki na wasiokuwa wao haifai kabisa kupewa zaka.

Mwisho

Mwisho napenda kuwausia waumini popote walipo kumcha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Aliye tukuka na kushikamana na ibada ya zaka, kutoa zaka si kupata hasara bali ni faida tupu mbele ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Na Zaka ni nguzo muhimu kuitekeleza katika Uislamu bali imetajwa sana pamoja na Swala. Kwa hiyo kuitekeleza nguzo hii ni kumsafisha mtoaji kutokana na sifa ya ubakhili na madhambi. Pia ni kutakasa mali yake na kuzidisha baraka kwa kutoa zaka, kuondoa chuki na uhasidi katika nafsi za wenye kupokea zaka, bali kuleta mapenzi kati ya tajiri na maskini.

Mwisho kabisa tunamuomba Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Atujaalie tuwe miongoni mwa wanaotekeleza ibada ya zaka, pia tunamuomba Ayabariki mali zetu, Atupe ujira mkubwa kwa tunachokitoa kesho akhera.





Vitambulisho: