islamkingdomface islamkingdomtwitte islamkingdominstagram islamkingdompinterest islamkingdomtumblr islamkingdomreddit islamkingdomvk


KUWATENDEA WEMA KWA WAZAZI WAWILI NA TAHADHARI YA KUWAASI


16971
wasifu
Haki ya wazazi wawili iko na inaendelea, na kukaa nao vyema ni lazima, hata kama wao ni makafiri, kwani kuwatenda wema haihusiani na kuwa wao ni Waislamu. Uislamu umeonya juu ya kuteta na wao maonyo makali, ukafanya kuteta na wazazi wawili ni miongoni mwa makubwa ya madhambi makubwa baada ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, bali ulifadhilisha kuwatumikia wazazi wawili juu ya kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu ambako ndio kilele cha Uislamu.
Khutba ya

Wazazi wawili wanayo haki kubwa kutoka kwa watoto wao, kama walivyo na haki watoto kutoka kwa wazazi wao. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Ameweka wazi kabisa haki za Pande zote mbili. Mwenyezi Mungu hakuwaachia wanadamu wajipangie wenyewe haki zao, bali Yeye Mwenyewe Amechukua jukumu la kuwapangia kila moja haki yake ili asipatikane na upungufu au dhulma katika kugawa hizo haki. Wazazi wana nafasi kubwa katika Dini ya Kiislamu. Wao ndio sababu ya kupatikana mtoto, baada ya kuvumila na kusubiri juu ya shida nyingi kisha kuzaliwa mtoto. Kwa kuvumilia kwao na kusubiri juu ya shida zote, wamepata cheo kikubwa mbele ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).

Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, mazungumzo yetu ya leo yataambatana kuhusu haki ambayo amelinganisha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) haki hiyo na haki yake katika maneno mengi katika kitabu chake kitukufu, nayo ni haki ya wazazi wawili. Jueni kwamba mafungamano makubwa baina ya mja na Mola wake ni kuumcha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) na kusimamia haki za wazazi na kusimamia haki za waja wake.

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى): وَاعْبُدُوا اللَّهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَبِذِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى) [النساء: 36]

{{Mwabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima}}.

Jueni waja wa Mwenyezi Mungu kwamba kuwafanyia wema wazazi wawili ni wajibu hata kama ni makafiri, imepokewa na Asma “ Amenijia mamangu na yeye ni mshirikina nikamshauri Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) kwa kumkata, Akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Mfanyie wema mamako]. Wema kwa wazazi haukatiki hata kama watakuamrisha kumkufuru Mwenyezi Mungu na kumshirikisha.

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَوَصَّيْنَا الْإِنْسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَى وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ14 وَإِنْ جَاهَدَاكَ عَلى أَنْ تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُمْ بِمَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ) [لقمان: 15]

{{Na tumemuusia mwanadamu kuwafanyia ihsani wazazi wake – mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumnyonyesha na kuja kumuachisha kunyonya katika miaka miwili- basi unishukuru Mimi na wazazi wako; marejeo yenu ni kwangu. Na wazazi wako wakikushurutisha kunishirikisha na yale ambayo huna ilimu nayo, usiwatii; lakini kaa nao kwa wema hapa duniani}}.

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu alitanguliza haki za wazazi wawili kuliko jihadi. Imepokewa Hadithi na ‘Abdillah Ibn Mas’oud Amesema: [Nimemuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu amali gani ni bora Mbele ya Mwenyezi Mungu? Akasema: Swala katika wakati wake. Akasema kisha ni amali gani? Akasema: kuwafanyia wema wazazi wawili. Nikasema kisha amali gani? Akasema: jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Imepokewa na Muawiya bin Jahim Amesema: Amekuja mtu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu akasema nataka kwenda jihadi, na nimekuja kukushauri. Akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) je una mama? Akasema ndio. Akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) jilazimishe na mama yako, kwani pepo iko chini ya miguu yake. Na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) anaomba kwa aliyepata wazazi wawili au mmoja wao na hakuingia peponi kwasababu yao basi mtu huyu amekhasirika].

Na visa vya wale watu watatu waliofunikwa na pango na hawakuweza kutoka akasema mmoja wao angalieni amali njema mliyomfanyia Mwenyezi Mungu, mumuombe Mwenyezi Mungu kupitia amali hiyo huenda Mwenyezi Mungu akatufariji, akasema mmoja wao: nilikuwa na wazazi wawili watu wazima na nilikuwa na watoto wadogo na nilikuwa nikiwachungia na ninapokamua nawanywesha wazazi wangu kabla ya watoto wangu, nilipokuja jioni na maziwa nimewakuta wamelala, nikaona vibaya kuwaamsha, pia nikachukia kumtanguliza mtoto wangu kabla yao na mtoto wangu alikuwa akilia na ilikuwa hivyo mpaka alfajiri, ewe Mwenyezi Mungu ukijua tendo langu hilo nikutaka radhi zako basi tufariji, Mwenyezi Mungu akawafariji mpaka wakawa wanaona mbingu.

Na katika kuwatendea wema ni kuwatii maadamu hujakhalifu amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ) [لقمان: 15]

{{Kaa na wao kwa wema hapa duniani}}. Na haki yao ni kuwapatia matumizi na kuwavisha ikiwa ni maskini, na kuwaombea Mwenyezi Mungu wakiwa hai na baada ya kufa Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) وَقَضَى رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِنْدَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُلْ لَهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُلْ لَهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا 23 وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُلْ رَبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا) [الإسراء23: 24]

 

{{Na Mola wako amehukumu kuwa msimuabudu yoyote ila Yeye tu. Na kuwafanyia wema wazazi. Kama mmoja wao akifikia uzee, naye yuko pamoja nawe, au wote wawili, basi usiwaambie hata Ah. Wala usiwakemee. Na useme nao kwa msemo wa heshima}}.

Imepokewa na Ibn ‘Umar kwamba yeye akitoka kuelekea Makkah alikuwa na punda na kilemba amejifunga nacho kichwani, siku moja alikutana na Bedui, akasema Bedui yule kumwambia Ibn ‘Umar Je, wewe si mtoto wa fulani? Ibn ‘Umar akasema ndio. Pale pale Ibn ‘Umar akampa punda yule Bedui ampande na kilemba ajifunge. Baadhi ya Maswahaba wakasema Mwenyezi Mungu akusamehe umempatia bedui huyu punda ambaye kwamba ulikuwa ukitembea naye na kilemba uliyokuwa umejifunga nacho. Akasema amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Bora ya wema ni kuunga mtu vipenzi vya babake baada ya kuondoka duniani].

Kubainisha Cheo cha Kuwatendea Wema Wazazi Wawili, Thawabu zake na Fadhila zake.

Enyi Waislamu kuwatendea wema wazazi wawili ni sababu ya kuingia peponi, je umepata kujua kisa cha Uweis Bin Annur Al-Qarni? Huyu ni mtu aliyesimuliwa na Mtume kisa chake na akaamrisha maswahaba zake kutaka dua kutoka kwake, na kukurubishwa kwa Mwenyezi Mungu na haikuwa alama yake isipokuwa kuponya, hadithi ambayo ameipokea Imam Muslim inaeleza kuwa ‘Umar alijiwa na pote kutoka Yemen akauliza jee kuna Uweis kati yenu? Mpaka alipokuja Uweis akasema wewe ndio Uwes? Akasema ‘Umar jee ulikuwa na ugonjwa wa ukoma ukapona isipokuwa sehemu kama ya shilingi, akasema ndio, akasema ‘Umar jee una mama? Akasema ndiyo. Akasema nimemsikia Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akisema: [Atakujieni Uweis na pote kutoka Yemen na alikuwa na ukoma na akapona ila sehemu ya shilingi na alikuwa mwema kwa mamake akimuapia Mwenyezi Mungu huwa jambo hilo ukiweza akuombee msamaha]. Akasema ‘Umar niombee msamaha na akamuombea ‘Umar msamaha.

Na Muhammad Ibn Sirin alikuwa akinyenyekea anapozungumza na mamake.

Hassan bin ‘Ali Ibn Hussein Zeinul ‘Abidin alikuwa akimfanyia wema mamake mpaka akaulizwa siku moja, kwa nini hatukuoni ukila sahani moja na mamako? Akasema naogopa kutangulia mkono wangu sehemu ambao kwamba jicho la mama limekwisha kutangulia, na hapo nitakuwa nimemuasi.

Na huyu Shureyh alikuwa ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa alikuwa akiwafundisha wanafunzi wanaokuja kutoka sehemu mbali mbali na mamake alikuwa akimtuma kwa kumwambia awapatie chakula kuku, basi husimama na kuacha kufundisha. Huu ni mfano wa watu wema waliotangulia, vipi hali ya barobaro wetu leo huenda mmoja wao kukosea heshima mzazi wake na kumridhisha rafiki yake. Nakuusieni kuwafanyia wema wazazi wenu na kwenda mbio kuwaridhisha wao.

Khutba ya pili

Ndugu zangu Waislamu kuwaasi wazazi wawili ni katika madhambi makubwa baada ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Je sikufahamishieni madhambi makubwa? Tukasema ndio ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, akasema ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kuwaasi wazazi wawili].

Imepokewa na Ibn ‘Umar (Radhiya Llahu ‘anhu) akisema, amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Watu watatu hawatoangaliwa na Mwenyezi Mungu, mmoja wao ni Mwenye kuwaasi wazazi wake wawili].

Kuwaasi wazazi wawili kuna namna nyingi:-

Kukunja uso unapokabiliana nao.

Kuinua sauti unapozungumza nao.

Kuwakata maneno yao kwa kuwakemea au kuwalazimisha rai yako kwao.

Kuwatizama kwa jicho la dharau.

Kuchelewesha kukidhi haja zao.

Tahadhari kuwatangulizia Wasiokuwa Wazazi Wawili kwa Kuwafanyia Wema.

Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Hapana dhambi ambayo adhabu yake huletwa kwa haraka kama kukata kizazi na dhulma]. Imepokewa kisa cha mtu mkubwa alimchukua babake katikati ya jangwa. Baba akasema: wanipeleka wapi mtoto wangu?. Mtoto akasema : umenichosha. Baba akasema: unataka nini? Mtoto: nataka kukuchinja umenichosha babangu. Baba: ikiwa hauna budi basi nichinje katika bonde lile. Mtoto: akasema kwa nini? Baba: nimemchinja babangu katika bonde lile lile, niuwe na utaona watoto wako watakuuwa katika bonde lile lile.

Mwisho

Ndugu katika imani, tujihadhari sana kutowafanyia wazazi wema. Adhabu yake ni kali sana na ni ya haraka kuadhibiwa hapa duniani na kesho akhera. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) Aliweka wazi suala hili kwa lengo la kumtahadharisha mwanadamu na maangamivu atakayo pata pindi akiwaasi wazazi wake. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Hakuna dhambi ambalo Mwenyezi Mungu Anatanguliza kumuadhibu mja wake hapa duniani kuliko kukata jamaa, na kumuwekea adhabu nyingine siku ya kiama]. Waja wa Allah, rudini kwa Allah kwa kumuomba msamaha kwa makosa yote tuliyo mfanyia. Na tuweke azma ya kuwafanyia wema wazazi wawili kama tulivyo fundishwa na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

Tunamuomba Allah Atukubalie ibada zetu na atuwafikishe kufuata Kitabu chake na Sunna za Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).





Vitambulisho: